Kwa mujibu wa Kitengo cha Kimataifa cha Shirika la Habari la Hawza, kikinukuu Shirika la Habari la Anadolu, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisema katika kujibu kauli za Netanyahu:
“Uongo ambao Netanyahu, mtaalamu wa mauaji ya kimbari, anautumia kuficha ukweli hauwezi kufunika wajibu wake kuhusiana na uhalifu mkubwa alioufanya.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Uturuki ilisisitiza katika taarifa yake iliyoandikwa kwamba; tuhuma zisizo na msingi, za uchochezi na zisizolingana na ukweli dhidi ya Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdoğan ni juhudi za Netanyahu na washirika wake za kuupotosha umma duniani.
Katika taarifa hiyo ilisemwa: “Uongo ambao Netanyahu, mtaalamu wa mauaji ya kimbari, anautumia kuficha ukweli hauwezi kuficha wajibu wake kufuatia uhalifu mkubwa alioufanya, Uturuki itaendelea kueleza ukweli kumhusu Netanyahu na washirika wake kwa lugha iliyo wazi zaidi, na itafanya juhudi kwa uthabiti ili kuwawajibisha mbele ya vyombo vya kimataifa vya mahakama kwa sababu ya vitendo vyao vinavyokiuka sheria na maadili ya kibinadamu.”
Cevdet Yılmaz: Kauli za Netanyahu Hazina Thamani Katika Dhamiri ya Binadamu
Cevdet Yılmaz, Makamu wa Rais wa Uturuki, alisema katika ujumbe wake: “Netanyahu, ambaye anashtakiwa kwa tuhuma za mauaji ya kimbari katika mahakama za kimataifa na ambaye kwa uzembe mkubwa ameweka eneo letu katika moto wa vita, hawezi kuficha uhalifu na madhambi yake kwa kutumia kashfa na tuhuma zisizo na msingi dhidi ya Rais wetu, kauli zake hazina thamani yoyote kwetu wala katika dhamiri ya wanadamu.”
Aliongeza kwamba; Jamhuri ya Uturuki itaendelea kutetea sheria, diplomasia, amani na mataifa yaliyodhulumiwa katika ngazi ya kikanda na kimataifa.
Kwa upande wake Akın Gürlek, Waziri wa Sheria wa Uturuki, pia alisema: “Kauli za dharau za Benjamin Netanyahu dhidi ya Rais wetu, wakati yeye mwenyewe amehukumiwa katika dhamiri ya pamoja ya wanadamu kwa sababu ya ukatili dhidi ya watoto, wanawake na raia wasio na hatia huko Gbaza, hazina thamani yoyote.”
Aliongeza kwamba; Netanyahu ni mtuhumiwa katika kesi inayohusiana na madai ya mauaji ya kimbari inayofuatiliwa na Ofisi ya Mwendesha Mashtaka ya Istanbul, na kwamba mashambulizi yake ya maneno dhidi ya Erdoğan ambaye anatetea heshima ya mwanadamu ni “mfano kamili wa kupotoka kwa uwezo wa kuhukumu na mantiki.”
Waziri wa Mambo ya Ndani: Serikali ya Netanyahu ni Alama Wazi ya Ukaliaji wa Mabavu Duniani Leo
Mustafa Çiftçi, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Uturuki, alisema katika kujibu matamshi ya Netanyahu: “Miitikio ya mara kwa mara ya serikali ya Netanyahu inayotuhumiwa kwa mauaji ya kimbari dhidi ya kauli za Rais wetu, inaonyesha wazi jinsi kauli hizo zilivyogusa kiini cha ukweli.”
Alisisitiza kwamba; serikali inayoua watoto, wanawake na raia huko Ghaza na ambayo imegeuza njaa na kiu kuwa silaha haiwezi kuzungumzia maadili, haki na haki za binadamu.
Çiftçi aliongeza: “Leo, alama iliyo wazi zaidi ya ukaliaji wa mabavu, upanuzi wa ardhi kwa nguvu, kuwafukuza watu kwa lazima na kupora ardhi duniani ni serikali ya Netanyahu.”
Kwa upande wake Alparslan Bayraktar, Waziri wa Nishati wa Uturuki, alisema: “Kauli za dharau za wale waliofanya moja ya mauaji makubwa zaidi ya kimbari katika historia huko Gaza dhidi ya Rais wetu, ambaye ni sauti ya dhamiri ya pamoja ya wanadamu, si chochote ila ni taswira ya kushindwa na kutoweza kwao.”
Kemal Memişoğlu waziri wa Afya nae alisema: “Kauli za mtu aliyeshambulia kwa mabomu hospitali za Ghaza na anayelishwa na damu ya watu wasio na hatia, dhidi ya Rais wetu ambaye ametumia maisha yake katika kuuhudumia ubinadamu ni mwonekano dhaifu wa hali ya kisaikolojia inayotokana na hisia za hatia.”
Aliongeza kwamba; Netanyahu atabaki katika kurasa za aibu za historia kama “uso wa uharibifu”, ilhali Erdoğan ataendelea kubaki kwa waliodhulumiwa wa dunia kama “ngome imara ya dhamiri ya kibinadamu”.
Ömer Çelik, msemaji wa Chama cha Haki na Maendeleo (AKP), alisema katika kujibu matamshi ya Netanyahu: “Netanyahu anasema kwamba jeshi la Israel ndilo lenye maadili zaidi duniani, huu ndio uongo mkubwa zaidi duniani, hakuna mtu ambaye hajaathiriwa na maradhi ya Uzayuni anayeweza kuliona jeshi lililofanya mauaji ya kimbari huko Ghaza kuwa la kimaadili.”
Aliongeza kwamba; mauaji ya kimbari huko Ghaza, mashambulizi dhidi ya Iran na mauaji yaliyofanyika Lebanon ni miongoni mwa “uhalifu usio wa kimaadili zaidi, usio na dhamiri zaidi na mkubwa zaidi duniani.”
Inafaa kutajwa kwamba Netanyahu aliandika katika ukurasa wake wa X akimwelekea Erdoğan: “Erdoğan, dikteta mwenye chuki dhidi ya Wayahudi ambaye amefanya mauaji ya kimbari dhidi ya Wakurdi, anaunga mkono shirika la kigaidi la Hamas, anawakandamiza wananchi wake mwenyewe na anawafunga wapinzani wake wa kisiasa gerezani, ndiye mtu wa mwisho kabisa anayepaswa kuifundisha serikali ya Israel masuala ya maadili.
Serikali ya Israel na Vikosi vya Ulinzi vya Israel (IDF), ambavyo ni jeshi lenye maadili zaidi duniani, vitaendelea na hatua zao madhubuti na zenye nguvu dhidi ya Iran na vikosi vyake vya washirika ambavyo vinatishia Mashariki ya Kati na dunia nzima.”


Maoni yako